TAMISEMI
KUKANUSHA TAARIFA ZA MITANDAONI
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), itawaajiri walimu wa masomo yote kama inavyofanywa kila mwaka baada
ya Bunge kupitisha bajeti ya Serikali.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na
Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mussa Iyombe alipozungumza na waandishi wa habari
kukanusha habari zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa serikali
imesitisha ajira za walimu.
Alisema taarifa hizo sio sahihi na kuwa serikali
itatoa ajira kama inavyofanywa kila mwaka baada ya kupitishwa kwa bajeti ya
mwaka 2016/17. “Ajira za walimu zipo. Bajeti ikipitishwa na wabunge, suala la
kuajiri walimu litaendelea kama ilivyokuwa miaka mingine,” alisema.
Taarifa za kwenye mtandao ambazo Serikali imesema si
za kweli zinasema kuwa utafiti uliofanywa na Tamisemi umebaini kuwapo kwa zaidi
ya walimu 7,988 wa masomo ya Sanaa na Biashara katika shule za msingi na
sekondari.
Aidha, taarifa hiyo inadai kutokana na ziada hiyo,
Serikali itasitisha ajira za walimu hao mpaka kutakapokuwa na uhitaji na badala
yake itaajiri walimu wa Sayansi na Hisabati mwezi Novemba mwaka huu na kuwa
walimu wa Sanaa na Biashara wajiingize katika masuala mengine ya kujipatia
kipato.
Iyombe amewataka wananchi kupuuza taarifa hiyo kwa
sababu haina ukweli na wala haijatolewa na ofisi yake. “ Napenda kujulisha umma
kuwa taarifa hiyo ni batili na imelenga kuchonganisha wananchi na Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli. Pia taarifa hizi zimelenga
kujenga hofu na chuki kwa walimu ambao wamehitimu masomo ya Sanaa na Biashara
ili waichukie serikali,” alisema.