Tuesday 13 September 2016

TAMISEMI KUKANUSHA TAARIFA ZA MITANDAONI



TAMISEMI KUKANUSHA TAARIFA  ZA MITANDAONI
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), itawaajiri walimu wa masomo yote kama inavyofanywa kila mwaka baada ya Bunge kupitisha bajeti ya Serikali.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mussa Iyombe alipozungumza na waandishi wa habari kukanusha habari zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa serikali imesitisha ajira za walimu.
Alisema taarifa hizo sio sahihi na kuwa serikali itatoa ajira kama inavyofanywa kila mwaka baada ya kupitishwa kwa bajeti ya mwaka 2016/17. “Ajira za walimu zipo. Bajeti ikipitishwa na wabunge, suala la kuajiri walimu litaendelea kama ilivyokuwa miaka mingine,” alisema.
Taarifa za kwenye mtandao ambazo Serikali imesema si za kweli zinasema kuwa utafiti uliofanywa na Tamisemi umebaini kuwapo kwa zaidi ya walimu 7,988 wa masomo ya Sanaa na Biashara katika shule za msingi na sekondari.
Aidha, taarifa hiyo inadai kutokana na ziada hiyo, Serikali itasitisha ajira za walimu hao mpaka kutakapokuwa na uhitaji na badala yake itaajiri walimu wa Sayansi na Hisabati mwezi Novemba mwaka huu na kuwa walimu wa Sanaa na Biashara wajiingize katika masuala mengine ya kujipatia kipato.
Iyombe amewataka wananchi kupuuza taarifa hiyo kwa sababu haina ukweli na wala haijatolewa na ofisi yake. “ Napenda kujulisha umma kuwa taarifa hiyo ni batili na imelenga kuchonganisha wananchi na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli. Pia taarifa hizi zimelenga kujenga hofu na chuki kwa walimu ambao wamehitimu masomo ya Sanaa na Biashara ili waichukie serikali,” alisema.

No comments: